#UTALII:Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesisitiza kuwa zoezi la kuhama kwa hiari kwa wananchi wa Ngorongoro linaendelea huku akisisitiza kwamba Serikali inafanya maboresho mbalimbali ili kurahisisha zoezi hilo.
Ameyasema hayo Septemba 12, 2024 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro katika Makao Makuu ya Ofisi za (NCAA) Wilayani Karatu Mkoani Arusha.
"Niseme tu kwamba zoezi la kuhama kwa hiari linaendelea na maboresho yanaendelea na kuna maeneo ya Kitwai, Kilindi na sehemu nyingine ambazo watu wanapenda kwenda wanaenda kwa hiari ". Amesisitiza Chana.
Amewataka askari uhifadhi kusimamia vyema zoezi hilo ili kurahisisha utekelezaji wake huku akiwataka kuendelea kufuata maelekezo mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi kama geti na vyoo vya wanafunzi.