DC KIGAMBONI NA UTARATIBU MPYA KUSHUGHULIKIA KERO ZA WANANCHI
Tarehe: 11 Sep, 2024
#DAR ES SALAAM:Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mhe.Halima Bulembo ameanza utaratibu mpya wa kusikiliza kero za wananchi mtaa kwa mtaa akiwa na lengo la kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi huku akiwataka watumishi wa Halmashauri kuhamishia ofisi zao mitaani ili kutoa huduma moja kwa moja.
Aidha ameeleza kuwa zoezi hilo ni tofauti kama ilivyozoeleka mwanzo kwa kuja kuweka mikutano ya hadhara na kusimama mtu moja mmoja na kuzungumza kero yake na kwamba katika awamu hii kila mwenye changamoto atasogea kwenye meza, atasikilizwa na kutatuliwa changamoto yake kama ambavyo angefika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya au mkuu wa idara.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wa mtaa wa Ferry Dkt. Khalid Sharifu na Bi Beatrice Samweli wakizungumza kuhusu utaratibu huo wa kushughulikia kero kwa kupongeza uamuzi uliochukuliwa na Mkuu wa Wilaya kwa kuwafuata wananchi na kutatua kero zao huku wakimuomba awatatulie changamoto ya huduma ya kivuko ili waweze kufanya shughuli zao kwa wepesi.
Aidha Mhe. Bulembo amewataka wananchi wa mitaa mingine kukaa tayari kwani kila mmoja atafikiwa na kero zitatatuliwa.
Awali ziara ya Mkuu wa Wilaya iliyopewa jina la mtaa kwa mtaa inatarajiwa kuifikia mitaa yote 67 iliyopo katika kata tisa zilizopo Manispaa ya Kigamboni.