National News

SERIKALI IMEENDELEA KUHAKIKISHA TIJA,USTAWI WATUMISHI AFYA

Tarehe: 11 Sep, 2024


#AFYA:Serikali kupitia Wizara ya afya imesema  itaendelea kuhakikisha tija na ustawi wa wauguzi, madaktari na watumishi wote wa sekta hiyo kupata stahiki zao pamoja na kuwasimamia na kufuatilia wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwa na lugha zenye staha kwa wagonjwa (customer care). 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Septemba 11, 2024 wakati akiongea na watumishi pamoja na wagonjwa akiwa kwenye ziara yake ya kukagua huduma zinazotolewa katika Taasisi ya Moyo ya Jakawa Kikwete (JKCI) Jijini Dar Es Salaam. 

"Afya ni usalama wa nchi, afya ni maendeleo ya nchi, afya ni jambo la msingi sana katika ustawi wa taifa, tunasema leo tumefikia uchumi wa kati ni kwa sababu tumeboresha afya za wananchi kwa hiyo ni lazima tusimamie vizuri maslahi ya watumishi lakini na utendaji wao." Amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa katika Sekta ya Afya hasa katika uwekezaji wa rasilimali watu pamoja na vifaa, vifaa tiba katika huduma za ubingwa bobezi. 

"Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka Mitatu Serikali imewekeza katika utoaji wa huduma za kibingwa ambapo nchi zaidi ya 20 zinakuja Tanzania kupata huduma hizo ikiwemo nchi ya Ujerumani." Amesema Waziri Mhagama.

Katika hatua nyingine Waziri huyo ameipongeza (JKCI) kwa huduma zinazotolewa za kiubunifu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema Taasisi hiyo kupitia Samia Outreach Program imeweza kufikia mikoa 16 na kwamba wameshawaona  wananchi elfu 17,000 na wengine na Taasisi hiyo kwa matibabu.