National News

WAFANYABIASHARA KIGOMA WAHIMIZWA MATUMIZI MIUNDOMBINU INAYOTEKELEZWA NA SERIKALI

Tarehe: 31 Jul, 2024


#HABARI:Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fursa zitokanazo na  uimarishwaji wa Miundombinu ya kutolea huduma za jamii unaofanywa na Serikali ya awamu ya Sita mkoani Kigoma kwa lengo la kufanya Mageuzi ya kibiashara kupitia uwekezaji.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipozungumza wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Biashara Mkoa wa Kigoma Leo Julai 31, 2024 uliofanyika katika Hoteli ya Lake Tanganyika, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Mazingira bora ya kibiashara ili kutimiza dhamira ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  ya kuufanya mkoa kuwa Kitovu cha biashara kwa ukanda wa Magharibi.

Ameeleza kuwa ili kuleta tija ya kiuchumi,  mabaraza ya biashara  yasitumike katika kutatua changamoto pekee bali kuweka mikakati ya pamoja katika kuibua fursa za kibiashara na uwekezaji ili kuinua Uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

"Iwapo mikutano ya wafanyabiashara na uongozi wa Serikali itafanyika mara kwa mara, itaondoa migogoro isiyo ya lazima na kuepusha migomo ya wafanyabiashara inayoweza kujitokeza kutokana na changamoto zilizopo kupata utatuzi kwa wakati" amesema Andengenye.

Ameendela kusisitiza kuwa,  katika kuimarisha Mazingira ya uendeshaji wa shughuli za kibiashara, serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya uchukuzi ikiwemo kufanya ukarabati wa meli za Mt. Sangara, MV. Liemba na MV. Mwongozo sambamba na ujenzi wa barabara zinazouunganisha mkoa na mikoa jirani kwa kiwango cha lami pamoja na kuunganisha mkoa katika Gridi ya Taifa ili kupata umeme wa uhakika.

Aidha Andengenye amesisitiza kuwa serikali itaendelea kupokea na kufanyia kazi maoni ya wafanyabiashara mkoani Kigoma  pamoja na kutatua changamoto zao kwa haraka ili kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara hao na kuwawezesha kufikia malengo waliyojiwekea kiuchumi. 

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab