TIC IMESAJILI MIRADI 707 HUKU AJIRA 226,585 ZIKITARAJIWA
Tarehe: 15 Jul, 2024
#HABARI:Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa Julai 2023 hadi Juni 2024 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 707 yenye thamani ya Dola Bilioni 6.561 za Kimarekani, ukilinganisha na miradi 369 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ikiwa na thamani ya Dola Bilioni 5.394 za Kimarekani.
Akitoa taarifa hiyo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TIC Gilliard Terry amesema katika miradi hiyo asilimia 38.19 inamilikiwa na watanzania na asilimia 42.86 inamilikiwa na wageni huhu asilimia 19.38 ikiwa ni miradi ya ubia kati ya watanzania na wageni.
Aidha, Terry amesema sekta ya uzalishaji viwandani ndio inayoongoza kwa usajili wa miradi ikiwa imesajili miradi 313 yenye thamani ya Dola Bilioni 2.462 za Kimarekani ikifuatiwa na sekta ya usafirishaji ikiwa imesajili miradi 128 yenye thamani ya Dola Bilioni 1.03.
Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira 226,585 ikilinganishwa na ajira 53,871 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.