National News

"MARUFUKU KUKAMATA BODABODA KWA KUVIZIA"- DC KIGOMA

Tarehe: 12 Jul, 2024


#KIGOMA:Waendesha Pikipiki (Bodaboda), Bajaji na Wafanyabiashara katika soko la Nazareti Manispaa ya Kigoma/Ujiji mkoani Kigoma wamemuomba mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kali kuwasaidia kutatua kero ya polisi kukamata pikipiki mara kwa mara kwa kuvizia katika soko hilo na kwamba limekithiri na kupelekea kutofanya kazi yao vizuri ya usafirishaji wa abiria wanaotoka na kungia na mizigo katika soko hilo.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma aliyefika sokoni hapo kwaajili ya kusikiliza kero mwenyekiti wa Soko hilo la Nazareti Bw. Sadock John amebainsha kwamba polisi wanaokamata vyombo hivyo vya moto wamefanya eneo hilo kama lango na kumepelekea kusuasua kwa biashara katika sokoni hapo.

“Tumekuwa na kero kubwa sana na Askari polisi kukamata  bodaboda kwenye soko hili...yani hapa ndiyo wamefanya kambi kwa muda mrefu sana  na ukiliangalia hili soko ni lango la kibiashara, tunauza matunda.....yaani matunda yanaharibika, kwahiyo usipouza siku moja maana yake kesho yake unamwaga, kwa mfano kama leo wafanyabiashara wangu hawajafanya biashara Soko limedorora..!! kwanini limedorora hakuna pikipiki zinazoleta wateja, hakuna pikipiki zinazoleta biashara”.Alieleza Mwenyekiti wa soko.

Akijibu kero hiyo mkuu wa Wilaya Salum Kali amewataka polisi kutumia njia ya kutoa elimu kwa madereva hao kabla ya kuwakamata huku akipiga marufuku kukamata kwa kuwavizia katika soko hilo kwasababu wengi wa madereva wanategemea kazi hizo kuendesha Maisha yao ya kila siku.

“Naomba kuanzia leo hapa mwisho, tusiviziane mtu anapokuja kwenye soko ndiyo anakuja kukamatwa kama ana kosa tumalizane hukohuko naomba tuelewane, hapa aje alete mzigo ukae sokoni.... hapa alete abiria anunue bidhaa”. Alieleza Kali.

Kwa upande wa wafanyabiashara wamemweleza mkuu wa Wilaya kuhusu kero yao ya kulipia ushuru wa jumla shilingi 8,000 kwa mwezi kuwa unawaumiza kutokana na kushindwa kuyamudu malipo hayo ya pamoja huku wakimuomba  awasaidie kurudisha utaratibu wa awali wa kulipa kidogokidogo shilingi 300 na kwamba utasaidia pia kapata kodi zaidi.

Akijibu hoja hiyo Kali amesema kuwa ataenda kulifanyia kazi na kwamba kuanzia tarehe 1 Agosti, 2024 atawapa majibu ili warejee katika utaratibu wa mwanzo wa kulipia ushuru kwa Shilingi 300 kwasababu hautaathiri ukusanyaji wa mapato katika Soko hilo.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab