National News

WASIMAMIZI WAZEMBE WA MAGATI KATIKA KULIPA MADENI KUSHUGHULIKIWA

Tarehe: 07 Jun, 2024


#KIGOMA:Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA), Ndugu Poas Kilangi, amesema kuwa ataanza kuchukua hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wasimamizi wa Magati ya Maji ambao wamekuwa wakizembea kulipa madeni kwa mamlaka hiyo. 

Kilangi ameyasema hayo wakati wa kikao na Wenyeviti wa Mitaa na wasimamizi wa Magati katika Kata ya Bangwe, Manispaa ya Kigoma Ujiji, na kuweka wazi msimamo wa Mamlaka dhidi ya malimbikizo ya madeni ya muda mrefu.

"Wananchi wanalipia gharama za kuchota maji, lakini changamoto kubwa bado iko kwa wasimamizi wa Magati ambao wamekuwa wakitumia fedha hizo badala ya kuzilipa kwa Mamlaka," alisema Kilangi.

Vilevile amesisitiza kuwa kuanzia sasa, kila msimamizi wa Magati atalazimika kulipia fedha wanazotoza kutoka kwa wananchi kila wiki kupitia namba maalum ya serikali ili kuepuka kulimbikiza fedha ambazo zingeweza kutumika katika kuendeleza na kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.

Sambamba na hayo ameongeza kwamba Mamlaka itafanya ukaguzi mara kwa mara kuhakikisha taratibu hizi zinafuatwa ipasavyo huku akiwataka viongozi wa serikali za kata, ikiwa ni pamoja na madiwani, maafisa utendaji, na wenyeviti wa mitaa, kusimamia kwa karibu huduma za maji kupitia Magati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na adha ya maji inapungua kwa Watanzania.

Katika kikao hicho, baadhi ya wasimamizi wa Magati na wenyeviti wa mitaa wamesisitiza umuhimu wa kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaokiuka taratibu za ukusanyaji wa fedha ili kuhakikisha nidhamu na uwajibikaji katika utoaji wa huduma ya maji.

Hatua hiyo ya (KUWASA) inaashiria dhamira yake ya kuhakikisha huduma ya maji inaimarika na inapatikana kwa wananchi kwa ufanisi zaidi, huku ikitoa onyo kwa wale watakaokiuka taratibu za malipo.