National News

SERIKALI IMEPAMBANA KUONDOA KATIKAKATIKA YA UMEME NCHINI

Tarehe: 07 Jun, 2024


#GEITA:Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko amesema  Serikali  imefanya kazi kubwa ya  kuhakikisha wanaondoa mgao wa umeme  kwa kuongeza vyanzo mbalimbali vya uzalishaji umeme na hivyo  kuondoa tatizo la kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo na kufanya kuwepo kwa umeme wa uhakika. 

Dkt, Biteko amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bukombe, Mkoa wa Geita ambapo pia ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga laini mpya ya Umeme kutoka Nyakanazi-Ushirombo na Kahama Bongwe hadi Bukombe ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa umeme katika  Wilaya ya Bukombe inaimarika.

Aidha  pamoja na ujenzi wa laini hizo za umeme, kutajengwa kituo cha kupoza Umeme Bukombe ili kuhakikisha wananchi wakiwemo wa Ushirombo wilayani Bukombe wananufaika na umeme wa uhakika.

"Umeme tunaopata Bukombe unatoka Bulyanhulu,  unapita Mbogwe na kuja  Bukombe ambapo  ukifika hapa unakuwa na nguvu hafifu na ikitokea hitilafu Bulyanhulu Bukombe pia inakosa umeme hivyo ni vema TANESCO ikajenga laini hizo mpya  ili wananchi wa Bukombe wapate umeme wa uhakika." Amesema Dkt. Biteko.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab