National News

WANANCHI KALALANGABO KUBORESHEWA HUDUMA YA MAJI

Tarehe: 04 Jun, 2024


#KIGOMA: Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA), Ndugu Poas Kilangi, amewaahidi wananchi wa Kijiji cha Kalalangabo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, kuwa uboreshaji wa chanzo cha maji na ufungaji wa pampu mpya utakamilika ifikapo Julai 15 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji hicho, Kilangi ameeleza kuwa jitihada muhimu zimefanyika, ikiwemo ununuzi wa Pampu mpya yenye thamani ya shilingi milioni 60 ambapo hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma ya maji kwa wananchi wa Kalalangabo inaimarika ili kutimiza malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha na kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.

"Nawaahidi kuwa, baada ya maboresho haya ambayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, wananchi wataweza kuanza kupata huduma ya maji majumbani, wakati huo huo, huduma ya Magati itaendelea kuwepo ili kutoa fursa kwa kila Mtanzania kutumia huduma ya maji safi na salama," alisema Kilangi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kalalangabo, Shamnte Ismail, alieleza kuwa serikali ya kijiji ina imani na (KUWASA) katika kuboresha huduma ya maji. 

"Tunaahidi ushirikiano katika hatua zote ili kusaidia wananchi ambao wamekuwa wakihitaji uongezaji wa huduma hii muhimu ya maji," alisema M/kt. Ismail.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao hicho wamepongeza hatua hiyo na kuomba uharakishaji wa ufungaji wa Pampu ya maji na miundombinu mingine ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo na kueleza kuwa utayari wao wa kutoa mchango wao katika kufanikisha zoezi la uboreshaji wa huduma ya maji.

Hatua hii ya (KUWASA) ni sehemu ya jitihada endelevu za kuboresha maisha ya wananchi wa Kalalangabo na maeneo mengine ya Kigoma, kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab