National News

"PANDENI MITI KATIKA MAZINGIRA YENU"- RC ANDENGENYE

Tarehe: 01 Jun, 2024


#KIGOMA:Wananchi mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza jitihada za kupanda miti katika mazingira yanayowazunguka hususani miti ya matunda ili kuendelea kuyatunza Mazingira na kuimarisha Afya zao kutokana na matunda hayo.

Akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya Mazingira ulioambatana na zoezi la usafi wa Mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni Kigoma lililofanyika leo tarehe 1Juni, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ambapo amesema kuwa suala la upandaji miti siyo lazima uwe na uchumi bali inahitajika dhamira ya dhati kwa kila mwananchi kuweza kutimiza lengo hilo na kutambua umuhimu wa utunzaji wa Mazingira.

“Hata ukipata Chungwa tuu zile mbegu ukazitunza ukazikausha na baadaye ukawa unazimwagilia hapo, unaweza kupata Miti ya matunda ya kupanda nyumbani kwako bila hata kuingia gharama ya kwenda kununua ule mche ulioko kwenye kilinda, kwahiyo kila mtu hili jambo halihitaji uwezo wa  kiuchumi, linahitaji tuu dhamira ya dhati katika kujua umuhimu wa utunzaji wa Mazingira”. Amesema Andengenye.

Kwa upande wake Afisa Mazingira Kanda ya Magharibi kutoka (NEMC) Bi.Regina Fidelis Kulwa amesema kuwa kampeni kuu ya wiki ya Mazingira kwa ujumla inahusiana na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika  ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba (NEMC) wanashirikiana na Halmashauri Pamoja na (NGOs) tofautitofauti kwaajili ya kusaidia baadhi ya Mazingira kuyawekea rutuba, kuyarejeresha ambapo pia wanashirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwaajili ya kupanda Miti ambayo ni rafiki kwa Mazingira.

Vilevile ameeleza kuwa (NEMC) wanawahamasisha Wananchi kupanda Miti  katika maeneo mbalimbali ambayo hayana Miti kabisa kutokana na uwepo wa biashara ya Hewa Ukaa na kwamba uwepo wa biashara  ya Kaboni (Carbon)kuna faida ambayo mwananchi anaweza kuipata kutokana na upandaji wa Miti.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab