#BUNGENI: Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 Bungeni Jijini Dodoma, amesema mapato ya jumla yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.5 mwaka 2022 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 36.
Mhe. Kairuki, amesema ongezeko hilo limeiwezesha Tanzania kuingia katika nchi 10 bora ikiwa ni ya 3 Barani Afrika na ya 9 Duniani ambazo mapato yake ya sekta ya utalii yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 28 ikilinganishwa na rekodi za mwaka 2019 kabla ya janga la UVIKO-19.
KATAVI:Mwanafunzi Luis Emmanuel (17) aliyekuwa anasoma katika shule ya Sekondari St. Mary's katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi amefariki dunia mara baada ya kunywa kemikali inayodhaniwa kuwa ni Ethanol katika Maabara ya shule hiyo wakiwa na wanafunzi wengine wawili wakifanya usafi katika Maabara hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kuhusiana na tukio hilo wanafunzi hao ambao walikuwa wanasoma kidato cha nne katika Shule hiyo walikuwa wakifanya usafi katika maabara ya kujifunzia masomo ya Sayansi kwa vitendo iliyopo shuleni hapo
Katika usafi huo walikuwa wakisimamiwa na Mwalimu John Mtafya ambaye alitoka nje kuendelea na shughuli nyingine za kimasomo na kuwaacha wanafunzi hao wakiendelea na usafi na baadaye walipoingia katika chumba cha kuhifadhia kemikali walichukua kemikali hiyo ya Ethanol na kuinywa na baadaye walipomaliza kufanya usafi waliendelea na masomo pasipo kusema chochote kuhusu kunywa kemikali hiyo.
Hata hivyo Wanafunzi wengine wawili Evangelist Deodatus (20) mpaka sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi huku Anastasia Zakayo (17) hali yake ikiendelea vizuri ambapo anaendelea na masomo yake.