SADC YASHAURIWA KUTAMBUA JUHUDI ZINAZOFANYWA MAENDELEO MAFUTA, GESI
Tarehe: 31 May, 2024
#HABARI:Naibu waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga ameishauri Sekretarieti ya (SADC) kutambua juhudi zinazofanywa na nchi wanachama katika kuendeleza program na miradi mbalimbali ya mafuta na gesi inayotekelezwa na nchi hizo na kuratibu katika utafutaji wa rasilimali fedha kama inavyofanyika katika eneo la Nishati ya umeme.
Mhe. Kapinga aliyaeleza hayo Luanda nchini Angola akimuwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko katika mkutano wa 42 wa Mawaziri wa Nishati na Maji wa Nchi za kusini mwa Afrika ( SADC) ambapo aliwaomba Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo kuunga mkono juhudi hizo zilizoanzishwa na Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naibu Waziri Kapinga pia alisema kuwa Tanzania imezindua Programu ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ya kuwasaidia Wanawake wa Afrika pamoja na Mkakati wake wa Kitaifa ikiwa na lengo la kuhifadhi mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kupunguza madhara ya kiafya, kupunguza mzigo wa mama na mtoto na ukatili wa kijinsia wakati wa kutafuta kuni na kuimarisha shughuli za kiuchumi na Kijamii ambapo ameelezea umuhimu wa Matumizi wa Nishati safi ya kupikia na matumizi mengine kwa Nchi za Afrika.
Mkutano huo wa Mawaziri ambao ulitanguliwa na vikao vya Makatibu Wakuu pamoja na wataalam ulijadili hali ya uzalishaji na upatikanaji wa umeme katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika, uendelezaji wa nishati ya mafuta na gesi pamoja masuala ya maji.
Aidha katika mkutano huo, Mhe. Kapinga aliongozana na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga pamoja na Kamishna Msaidizi wa Mafuta na Gesi Mha. Joyce Kisamo kutoka Wizara ya Nishati.