National News

HEDHI SALAMA KIKWAZO MAENDELEO YA WASICHANA

Tarehe: 29 May, 2024


#KIGOMA:Changamoto ya hedhi salama kwa watoto wa Kike katika shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo vya ufundi katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa kikwazo katika maendeleo ya msichana Kiafya na ustawi katika maendeleo ya Jamii 

Akizungumza katika Uzinduzi wa Mradi wa Binti pamoja na madhimisho ya siku ya Hedhi salama duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 28 Mei,Mkurugenzi wa AfriCraft Nchini Kelvin Nicholaus amesema vyuo vya ufundi vimekuwa vikisahaulika kupewa elimu ya upatikanaji Hedhi salama jambo ambalo limewasukuma  kutoa elimu ya uboreshaji wa taulo za kike. 

“Tunalenga sana kwenye vituo vya Elimu ya Ufundi katika mikoa Saba hapa Tanzania ikiwemo mkoa wa Kigoma, lemgo lingine kuu kwanini tunaenda kwenye vyuo vya ufundi  kwasababu wana ujuzi kwenye mausla ya ushonaji na masuala mengine  pia ya ujuzi”. Alisema Nicholas.

Akimuwakilisha Afisa Elimu sekondari, Afisa Elimu Maalum Manispaa ya Kigoma Ujiji Shingwa Hamis amesema mahitaji ya Taulo za kike katika shule za Manispaa hiyo ni makubwa yakiendana na changamoto ya ukosefu wa Vyumba vya kubadilishia Taulo katika shule hizo.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo ambaye alimuwakilisha mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Albert Mwesiga amesema licha ya kuwa ni suala la kibaolojia lakini wamelenga katika kumuinua na kumuwezesha Mtoto wa Kike kupitia Hedhi salama 

“Uwezeshwaji huu umejikita katika mambo makuu manne, jambo la kwanza kutoa elimu ya Afya kuhusu Hedhi salama kwa mabinti zetu lakini pia, uimarishwaji wa miundombinu kwenye Vyuo vya Ufundi, ugawaji wa sodo kwa Wanachuo, lakini pia mradi huu unalenga kuwawezesha vikundi vya akina mama wajasiliamali, kuwapa mafunzo, vifaa vya ushonaji wa Taulo za kike pamoja na Mashine”. Ameeleza Dkt. Mwesiga.

Mradi huo unatarajia kuwafikia zaidi ya wanafunzi wa kike elfu 12 pamoja na Vyuo 15 katika mikoa 7 ya Tanga, Kigoma, Dar es salaam, Morogoro, Rukwa, Lindi na Zanzibar, na  Maadhimisho hayo yameambatana na Kauli mbiu isemayo “Pamoja kwa Hedhi Rafiki Ulimwenguni “huku kauli mbiu ya Mradi ikiwa ni “Uwezeshwaji wa msichana kupitia Hedhi salama”.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab