WAPIGA KURA WAPYA LAKI 224,355 KUANDIKISHWA KIGOMA
Tarehe: 29 May, 2024
#INEC:Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajia kuawandikisha wapiga kura wapya 224,355 mkoani Kigoma katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika mkoani Kigoma tarehe 01-07 Julai, 2024 kwa muda wa siku 7.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhan Kailima amesema kuwa wapiga kura hao ni ongezeko la asilimia 21.50 ya wapiga kura milioni 1,043,281 waliopo kwenye Daftari mkoani Kigoma na kwamba tume hiyo imeuchangua mkoa Kigoma kufanyia uzinduizi huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza katika uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura kwa mwaka 2019/2020 pamoja na mwamko mkubwa katika kushiriki hamasa za siasa.
”Tunategemea baada ya kukamilisha daftri la mkoa wa Kigoma na matarajio haya linaweza likawa na watu Milioni moja,laki mbili sitini na saba, miasita thelasini na sita”.Amesema Bw.Kailima.
Kuhusu idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura, Bw. Kailima amesema katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka huu kutakuwa na jumla ya vituo 40,126, ambapo kati ya vituo hivyo vituo elfu 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar na kuongeza kuwa kwa Mkoa Kigoma vituo 1,162 vitatumika kwenye uboreshaji wa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 69 katika vituo 1,093 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
“Vituo vilivyoongezeka ni vituo 2,312, na kwa mkoa wa Kigoma vituo vinavyotumika ni vituo 1,162, na vimeongezeka vituo 69 na wakati wa uboreshaji kwa mwaka 2019/2020 vilikuwa vituo 1,093”. Ameeleza Bwn.Kailima.
Hata hivyo uboreshaji huo wa Daftari utatanguliwa na uzinduzi wa zoezi hilo utakaofanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa na baada ya mkoa wa Kigoma zoezi hilo litaendelea katika mikoa mingine ya Katavi, Rukwa pamoja na Tabora.