WANANCHI WTAKIWA KUTUNZA MIUNDOMBINU YA MAJI CHANZO BUBANGO- CHANKELE
Tarehe: 29 May, 2024
#KIGOMA:Wakazi katika vijiji vya Chankele na Bubango wilayani Kigoma wametakiwa kutunza miundombinu ya chanzo cha maji cha Bubago-Chankele ili kuepuka uharibifu wa chanzo hicho na kusababisha ukosefu wa huduma hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipofanya ziara ya kikazi katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma ambapo ametembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi zilizopo Kamara, mradi wa sekondari ya Msimba day, Mradi wa chanzo cha maji Bubango-Chankele, ujenzi wa hospitali ya wilaya pamoja na ujenzi wa ofisi ya mkurugenzi iliyopo kata ya Mahembe.
Amesema chanzo hicho cha maji cha Bubango-Chankele kimerebishwa na kupanuliwa kwa gharama ya shilingi milioni 900 ambapo kinahudumia watu zaidi ya 9000 hivyo iwapo kitaharibika kitasababisha usumbufu kwa watumiaji na hasara kwa serikali.
Ili kuhakikisha chanzo hicho kinakuwa salama, Andengenye amewataka watendaji wa wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) kushirikiana na wananchi kuhakikisha hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazofanyika ndani ya Mita 60 katika vyanzo vya maji.
Amesema maagizo hayo yanalenga kulinda vyanzo na miundombinu mingine ya maji liyowekwa kwaajili ya kuhudumia wananchi sambamba na kuthamini pesa zilizotolewa na serikali kwaajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji.
Amesema ni jitihada za kila mmoja kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani kwa kuondokana na kuchota maji kutoka kwenye magati ambapo kwa kijiji cha Chankele yapo magati 16 na Bubango yapo magati 19 yanayotoka maji na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo akiwa nyumbani kwake.
Amefafanua kuwa bado yapo maeneo yanayohitaji huduma za maji ndani na nje ya mkoa wa Kigoma na hivyo ni muhimu kutunza miundombinu hiyo ili fedha zilizopo zikagharamie miradi mingine.