National News

TANZANIA KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA MAZURI KWA WAWEKEZAJI

Tarehe: 23 May, 2024


#HABARI: Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hasa kupitia sekta ya viwanda Ili viweze kuchangia katika kuongeza fursa mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na ajira, fedha za kigeni kwaajili ya kuchangia na kukuza uchumi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wilayani Mkuranga, Mkoani Pwani wakati akizindua kiwanda cha Fortune ambacho ni chakwanza kwa ukanda wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambacho kinazalisha saruji nyeupe kwa ajili ya ujenzi ambapo  uwezo wake wa kuzalisha  Kwa siku ni tani 200.

Sambamba na hayo Naibu Waziri huyo alieleza kuwa kuwekeza nchini Tanzania ni sehemu salama na yenye mazingira yaliyoboreshwa ambayo kila mwekezani ataweza kunufaika pamoja na  wananchi kwa ujumla na kwamba uwekezaji huo ni sehemu ya kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi.

Vilevile serikali imezitaka halmashauri nchini kuendelea kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo rafiki kwa uwekezaji na wawekezaji kwa lengo la kuifikia azma ya serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji.

Katika hatua nyingine alisema kuwa serikali itashirikiana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho zinavuka mipaka ya nchi na kufika hata katika soko huru la Afrika.