National News

"TEKELEZENI MAPENDEKEZO YA TUME HAKI JINAI"- DKT. MPANGO

Tarehe: 18 May, 2024


#HABARI: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwepo kwa mfumo imara, wenye kuzingatia haki na misingi ya utawala bora katika kuwahudumia wananchi.

Ametoa kauli hiyo tarehe 18 Mei 2024 wakati akifungua warsha ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya 'Tume ya Haki Jinai' iliyofanyika ukumbi wa Kambarage, Dodoma.

Ameongeza kwamba nia ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuleta mapinduzi ya kifikra na mabadiliko ya kimfumo katika utendaji wa taasisi za 'Haki Jinai' hapa nchini.

Dkt. Mpango amewataka Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kutekeleza ipasavyo mapendekezo ya 'Tume ya Haki Jinai' kwa kuwa wananchi wameonesha hitaji la mabadiliko katika utendaji wa taasisi za haki jinai ili kuongeza uwezo na kuhakikisha haki inatendeka.

Dkt. Mpango amesema serikali imefanya jitihada na kutumia rasilimali nyingi katika kuboresha huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala hivyo ameagiza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Ujenzi kushirikiana ili kusimamia uanzishwaji wa ofisi za vyombo vya utoaji haki katika maeneo hayo.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab