"VIONGOZI TOENI TAARIFA KWA WANAHABARI"-RC ANDENGENYE
Tarehe: 15 May, 2024
#KIGOMA:Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ametoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wa Taasisi mbalimbali za serikali kuzingatia wajibu wao wa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari ili wananchi waweze kufahamishwa taarifa mbalimbali katika maeneo yao.
Andengenye ametoa maelekezo hayo katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Kigoma yaliyofanyika katika wilaya ya Kigoma akiwa mgeni rasmi huku akipongeza hatua ya klabu hiyo kuanzisha mahusiano ya ujirani mwema na jumuiya ya uandishi wa habari katika mikoa ya Burundi iliyo jirani na mkoa wa Kigoma na kwamba itachochoea waandishi wa habari kukua kimataifa kutokana na kubadilishana uzoefu baina ya pande zote mbili na kuchochea maendeleo kwa wananchi.
Aidha mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Pamoja na changamoto zinazoikumba tasnia ya habari bado waandishi wa habari wanao wajibu mkubwa kuendelea kuutangaza mkoa wa Kigoma na kutoa taarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi hususani athari za mvua katika mwaka huu ambazo zimeleta athari kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini ukiwemo mkoa wa Kigoma.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania Deogratius Nsokolo wakati akisoma risala kwa mgeni rasmi amesema kuwa moja kati ya changamoto wanayokumbana nayo waandishi wa habari mkoani Kigoma ni Pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali kutoonesha ushirikiano pale wanapofuatwa na waandishi wahabari ili kutoa taarifa kwa mustakabali wa wananchi na mkoa kwa ujumla na kuomba viongozi hao kutoa ushirikiano na kuacha kuwachukulia waandishi wa habari kama maadui.