National News

TIC, CMA WAINGIA MAKUBALIANO UTATUZI MIGOGORO

Tarehe: 03 May, 2024


#HABARI: Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) wameingia makubaliano ya ushirikiano ili kutatua changamoto za wawekezaji zinazotokana na migogoro ya wafanyakazi ili kudumisha uhusiano mwema mahala pa kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa (TIC) Gilead Teri amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuwapa wawekezaji uhakika wa mashauri yao kuweza kutatuliwa kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa (CMA) Usekelege Mpulla amesema makubaliano hayo yatasaidia kuendeleza Sera Bora za utatuzi wa migogoro nchini na kuendeleza sera bora za ajira ambazo zinaweza kusaidia kuzuia migogoro ya wafanyakazi au kuitatua kwa njia inayowajali wafanyakazi na wawekezaji.

Mashirikiano hayo yanatarajiwa kuanzisha mfumo wa namna bora ya utekelezaji wa makubaliano hayo ambapo kunatarajiwa kuwa na maofisa maalum watakaokuwa wanasimamia mchakato wa Utatuzi wa migogoro na hivyo kuharakisha mchakato wa kutatua migogoro hiyo kwa wawekezaji.

Vilevile  Mpulla amesema kwa sasa migogoro ya wafanyakazi imeendelea kupungua hadi kufikia migororo 5900 mwezi Februari mwaka 2024 ukilinganisha na migogoro 179,663 mwaka 2022 ambapo migogoro mingi inayowasilishwa ni ya madai ya kuachishwa kazi bila kufuata sheria.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TIC amesema kuanzisha kwa mashirikiano hayo kumefika wakati muafaka ambapo serikali ya awamu ya sita imejikita katika kutatua kero za wawekezaji ambapo kero kubwa mojawapo ni migogoro ya wafanyakazi na kwamba mfumo wa Kusikiliza Malalamiko kwa haraka kunatarajiwa kudumisha uhusiano kwani migogoro yao itatutuliwa kwa njia ya haki na inayoheshimu pande zote.

Kwa kufanya kazi kwa pamoja (TIC) na (CMA) wanatarajia kujenga mazingira bora ya kazi yanayostawisha ushirikiano, ufumbuzi wa migogoro kwa njia za amani, na kuboresha utendaji na ufanisi wa miradi ya uwekezaji inayowekezwa hapa nchini hivyo kuongeza ajira na kujenga uchumi bora.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab