#MEI MOSI:Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeadhimisha siku ya wafanyakazi duaniani 2024 (Mei Mosi) kwa kutoa matibabu bure kwa watoto zaidi ya 150 wenye matatizo ya mifupa na viungo.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Mifupa na Majeruhi MOI Dkt. Anthony Assey amesema kambi hiyo imefanikiwa kwa wazazi kujitokeza kwa wingi kuwaleta watoto wenye matatizo hayo huku taaarifa za awali zikibaini watoto wengi huchelewa kupelekwa hospitali.
“Matatizo mengi ni ya mfupa mrefu wa mguu, mkono na paja, mguu kifundo na kuna baadhi ya watoto hawana kabisa mfupa wa mguu, lakini pia wapo wenye matatizo ya nyonga” amsema Dkt. Assey na kuongeza kuwa
“Matibabu yametolewa bure, isipokuwa kwa wale wenye bima za afya tumewaingiza katika mfumo wa matibabu kupitia bima zao kwasababu hii kambi ni ya siku moja yaani leo tu lakini matibabu ya mifupa yataendelea, na kwa wale ambao hawana uwezo tumeweka utaratibu wa wao kuendelea kupata huduma”
Meneja wa huduma za upasuaji wa mifupa kwa watoto, daktari bingwa mbobezi Dkt. Bryson Mcharo amesema lengo lilikuwa kuwaona wagonjwa 100 hadi 200.
“Wengi wa watoto tuliowaona ni wa matege na mguu mmoja mrefu mwingine mrefu kimsingi watoto tuliowaona ni watoto ambao tulikuwa tunawahitaji ila wamechelewa kufika hospitalini ...tuungane kutokemeza ulemavu unaozuilika kwa watoto kwa kuwawahisha hospitali watoto hao” amesema Dkt. Mcharo
Taasisi ya MOI imetoa huduma hizo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi duania (Mei Mosi) 2024 ambapo huduma za kidaktari bingwa na bobezi zimetolewa kwa watoto wasio na uwezo.