#DAR ES SALAAM:Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wamekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa madereva mbalimbali nchini katika kikao kazi chenye lengo la kujadili changamoto ambazo wanakutana nazo wanapokuwa barabarani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Mizani TANROAD makao makuu, Mhandisi Japhet Kivuyo, alisema kikao hicho kimewashirikisha Taasisi mbalimbali za udhibiti za serikali ikiwemo LATRA, Jiji, Mkoa wa Dar es Salaam, Menejimenti ya Mkoa wa Dar es Salaam, ili kuhakikisha kwamba changamoto zote ambazo zitatolewa, ziweze kuwa na majibu.
Alisema baada ya kikao hicho ambacho kitapunguza changamoto nyingi ambazo madereva wanakutana nazo barabarani, anaamini madereva hao wataenda kuwa mabalozi wema katika kutenda kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na serikali.
"Tunategemea kwamba baada ya kikao hiki tutakuwa tumepunguza changamoto ambazo madereva wanakutana nazo barabarani na wao wataenda kuwa mabalozi wema katika kutenda kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ambazo zimeekwa na serikali"
Mhandisi Kivuyo alizitaja baadhai ya changamoto ambazo madereva hao wameziwasilisha ambazo ni pamoja na changamoto ya 'Wrong Parking' ambayo madereva wengi wamekuwa wakikumbana nayo na kupelekea kuchajiwa pesa pale wanapokamatwa.
Naye afisa Usajili na uthibitishaji wa madereva-LATRA Jerive Malaki alisema changamoto kubwa upande wa madereva ni elimu kutowafikia sawa sawa hivyo wanaendelea kutoa elimu na kuwataka madereva hao kwenda shule ili wapate elimu Kisha wathibitishwe na LATRA kwani udereva ni Taaluma na ni kazi kama kazi nyingine.
"Dereva ambaye atakuwa hajathibitishwa atakuwa amevunja sheria na anayevunja sheria anastahili adhabu na anakosa sifa za dereva anayestahili kuwa barabarani maana yake ni kwamba amekuwa amepungua katika baadhi za vigezo, kwa sasa tunaendelea kutoa elimu na kuendelea kuhamaisha na LATRA tumeshafungua vituo vya mitihani katika mikoa 18, katika mwaka huu wa fedha June 30, tuna mpango wa kufikia nchi nzima, na baada ya kufika nchi nzima, tutaweka tarehe ya ukomo kwa wale ambao watakuwa hawajafikia vigezo ambavyo vinatakiwa kwa mujibu wa sheria tutachukua hatua" Alisema
Kuhusu barabara inayotoka Kimara-Kibaha ambayo imekuwa na changamoto ya vituo vya daladala na Taa, Msimamizi wa Idara ya Mipango kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Clever Akilimali, alisema kuwa sehemu kubwa limeshakamilika lakini zipo sehemu ambazo hazijakamilika hasa katika kufunga Taa za usalama barabarani ambapo vyote vinafanyika katika mwaka huu wa fedha.
Aidha Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva Tanzania, Hassan Dede, alizitaja changamoto wanazokumbana nazo barabarani ikiwemo eneo la parking kuwa Si rafiki hasa wanapotoka nchi mbalimbali kuingia Jijini Dar es Salaam, lakini pia elimu waliyoianzisha LATRA ambapo tayari dereva anakuwa ameshasoma NIT huku LATRA wakiwataka madereva hao kwenda tena shule na kufanya mitihani ambayo alishaifanya NIT.
Kwa upande wake Mratibu Mwandamizi wa Polisi, Wakili wa serikali, mwanasheria kikosi Cha usalama barabarani (SSP), Deus Sokoni, alisema wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa madereva wasiotii sheria ikiwemo adhabu ya kufutiwa leseni ya udereva kwa kipindi Cha miezi mitatu-sita, kufikishwa mahakamani kwa kurudia kosa zaidi ya mara Moja na kuhukumiwa kwa rejea ya sheria za nchi lakini pia kuzuiwa leseni yake.