National News

DKT. BITEKO ASISITIZA UMUHIMU ELIMU MAHALA PA KAZI

Tarehe: 28 Apr, 2024


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko mewataka waajiri kwa kushirikiana na wadau wanaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza usalama mahala pa kazi na kuwawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira rafiki na hivyo kukuza uzalishaji na kupunguza gharama za uzalishaji.
 
Dkt. Biteko amesema hayo leo  28 Aprili,2024 Jijini Arusha katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa kazi Duniani.
 
 " Niwatake waajiri na waajiriwa kuhakikisha usalama mahali pa kazi, mtu wa kwanza kujali usalama wake ni mwajiriwa, ukiona mtambo hauko salama toa taarifa kwa mwajiri wako; hapa hautaonekana umegoma bali ni kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama ", amesema Dkt. Biteko.
 
Aidha Dkt. Biteko ameitaka OSHA kwa kushirikiana na wadau katika masuala ya usalama mahali pa kazi kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na mazingira yatakayowawezesha kuwa salama na kupata furaha na matumaini kisha kupata ari ya kuendelea kufanya kazi na kuongeza ufanisi kazini huku akiihumiza kuendelea kutoa elimu kuhusu wa usalama mahali pa kazi badala ya mfumo wa kizamani ambapo mwajiri na mwajiriwa walikuwa wakiogopana na kuhofiana kutokana na kufanya kazi za “KIPOLISI”
 
Pia amewataka Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa na mkakati wa upandaji miti na hatua nyingine za kukabiliana na madhara ya tabia nchi kama vile kuhifadhi vyanzo vya maji.
 
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobasi Katambi akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inashirikiana ILO kuhakikisha Tanzania inazingatia usalama na afya mahala pa kazi.
 
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa wafanyakazi ni wadau muhimu katika kufikia malengo ya taifa hivyo tukio hilo lina lengo la kuhamasisha kuhusu usalama mahala pa kazi ili kukuza uwekezaji na mafanikio yanayotarajiwa katika nchi.
 
 "OSHA tutaendelea kusimamia majukumu yetu kwa mustakabali wa Taifa letu na tutaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa usalama na afya mahala pa kazi", amesema Bi. 
 
Hata hivyo Mkurugenzi wa Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bi. Caroline Mugalla amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inaeleza umuhimu wa kuchukua taadhari ili kulinda afya za wafanyakazi. 
 
 "Naipongeza Serikali kwa kuridhia mikataba miwili ya mchakato huu unaendelea kupitia makubaliano ya pamoja baina ya Wafanyakazi na Serikali ili kuleta ufanisi mahali pa kazi na ILo tunaahidi kutoa ushirikiano kwao" amesema Bi.Caroline.
 
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri (ATE) ametoa wito kwa Serikali na Waajiri kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa inayozingatia usalama na afya mahala pa kazi huku mwakikishi wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bi. Juliana Mpanduji akisema kuwa TUCTA itaendelea kushirikiana na Serikali, OSHA na ATE ili kulinda nguvu kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.