National News

WATOTO 100 WENYE VICHWA VIKIBWA, MGONGO WAZI KUGHARAMIWA MATIBABU NA RAIS SAMIA

Tarehe: 21 Apr, 2024


MATIBABU WATOTO 100 WENYE VICHWA VIKUBWA, MGONGO WAZI KUGHARAMIWA NA RAIS SAMIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Dkt. Samia Suluhu Hassan atagharimia matibabu ya upasuaji na utengamao kwa watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi yatakayofanyika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).

Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amebainisha hayo leo Aprili, 21, 2024 alipotembelea Taasisi ya MOI kwa ajili ya kuwajulia hali watoto 25 waliofanyiwa upasuaji. 

Amesema Rais Dkt. Samia ameguswa na tatizo hilo na ameamua kugharamia matibabu ya watoto 100 zaidi ili kuepusha madhara na ulemavu unaoweza kusababishwa na kuchelewa kufanyiwa upasuaji.

"Mheshimiwa Rais Samia amenielekeza, nilete pesa kwa ajili ya watoto 100 ambao watafanyiwa upasuaji  wa kichwa kikubwa na mgongo wazi  bure kwa gharama za Rais Samia  Suluhu Hassan". Amesema Ummy.

"Kwahiyo Prof. Makubi wasilianeni na ASBATH kujua watoto hawa ndani ya wiki moja mbili wizara italeta hizo fedha za kugharamia matibabu au upasuaji na huduma za utengamao kwa watoto 100 kutoka kwa Rais wetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan” ameeleza Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy ameipongea taasisi ya MOI kwa kutoa matibabu ya watoto hao na MO Dewji Foundation kwa ufadhili wa matibabu ya watoto 50, huku akiwataka wadau kuendelea kujitokeza kusaidia wengine.

“Kubwa nataka kutoa wito kwa wazazi wenzangu kwa wale wenye watoto wenye changamoto hii ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wasiwafiche watoto hao, wahakikishe wanapeleka kliniki ili wapate ushauri wa kitaalam” amesisitiza Waziri   Ummy.

Kwa upande wake daktari bingwa mbobezi wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu MOI, Dkt. Hamisi Shabani amesema tatizo la vichwa vikubwa linaweza kuzuilika kwa kuhakikisha wanaume wanawalisha wake zao vyakula vyenye madini ya Frolic Acid na kuwawahisha kliniki kwa wale wenye tatizo hilo.

Naye mwenyekiti wa chama cha wazazi na walezi wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBATH) amesema kwa sasa chama hicho ina orodha ya watoto 200 wanaohitaji matibabu lakini kutokana na ukosefu wa fedha wapo majumbani huku wachache wakihudhuria klinik za watoto wa matatizo haya.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab