National News

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA SEKONDARI BUGENE

Tarehe: 21 Apr, 2024


#HABARI: Serikali imeahidi kujenga Mabweni mawili pamoja na kukamilisha ujenzi wa bwalo katika Shule ya Sekondari Bugene wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ili kuendelea kuboresha mazingira ya Wanafunzi kujifunza na kufundishwa.

Hayo yameleezwa Aprili 19, 2024 na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati akizungumza kwa njia ya simu na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Elimu), Dkt. Charles Msonde wakati wa mahafali ya kidato cha sita katika Shule hiyo.

"Katika Ujenzi wa bwalo niwashukuru Wazazi kwa mchango wa ujenzi wa msingi wa Jengo, Mchango wangu katika ujenzi huu ambao unahitaji mabati 519, Ofisi ya Mbunge itagharamia", amesema Waziri Bashungwa.

Bashungwa amesema Shule ya Sekondari Bugene imekuwa ikifanya vizuri katika taaluma hivyo Serikali itahakikisha inaweka mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishwa ili ufaulu uongezeke kimkoa na kitaifa.

Naye, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuinua Sekta ya Elimu nchini, hivyo ataliwasilisha suala hilo kwa  Waziri wa TAMISEMI ili ujenzi wa bwalo na Mabweni mawili uanze.

 "Haya uliyonieleza nitamwambia Waziri Mchengerwa, na najua hata Mheshimiwa Rais ndio mkakati wake wa kuinua Sekta ya Elimu nchini, kwa hiyo mabweni hayo lazima tuyajenge ili watoto wetu wasome vizuri" , Amesema Dkt. Msonde.

Kuhusu Ujenzi wa Bwalo, Dkt. Msonde amewapongeza wananchi kwa kujitoa na kuanza ujenzi na amemuagiza Mhandisi wa Halmashauri kufanya tathmini ya vifaa vinavyohitajika katika ujenzi ili Serikali iunge mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa bwalo.