Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni-Kigoma kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo tarehe 16 Aprili,2024 imeanza kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya matatizo ya moyo ambayo inafanyika katika hospitali hiyo ya rufaa.
Katika kambi hiyo ya siku tatu ambayo imeanza leo ambapo inatarajiwa kumalizika tarehe 18 Aprili, 2024 na yanahusisha uchunguzi na matibabu ya matatizo ya moyo inayo julikana kama Dkt. Samia Suluhu Hassan Tiba Mkoba, na wataalamu Pamoja na madaktari bingwa bobezi kutoka Taasisi hiyo ya Moyo Jakaya Kikwete wanatoa huduma katika Hospitali hiyo.
Dkt. Eva Wakuganda ambaye ni daktari bingwa wa moyo Upande wa Watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete amesema mpaka sasa wamefanya huduma hiyo katika mikoa takribani 13 wakiwasaidia wagonjwa wapatao 11,254 huku Kigoma ikiwa ni Mkoa wa 14 kufikiwa na huduma hiyo.
Pia Dkt. Eva ameeleza kuwa huduma hiyo ni endelevu kutokana na Taasisi hiyo kuwa na malengo ya kuwafikia wananchi wote ambapo pia ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita Chini ya Mh.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya kwa kununua vifaa tiba Pamoja na kuendelea kuwasomesha wataalamu katika kada ya Afya.
Kwa upande wake Dkt.Frank Sudai ambaye ni Mratibu wa Huduma za Afya Mkoa wa Kigoma ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo Jirani kutumia fursa hiyo ya kufika hospitalini hapo kutokana na huduma hiyo kusogezwa karibu, ambapo pia ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya Pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kusogeza huduma hiyo kwa wakazi wa Kigoma .
Naye Dkt.Boniphace Kilangi kwa niaba ya Mganaga Mfawidhi Hospitali Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni - Kigoma Dkt. Stanley Binagi awatoa wito kwa wananchi wa Kigoma kujitokeza kupata matibabu kwani imepunguza gharama ambazo zingetumika kuifuata huduma hiyo.