National News

PINDA AMSHUKURU RAIS SAMIA UJENZI MIUNDOMBINU YA UMEME

Tarehe: 11 Apr, 2024


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda amemshukuru Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi. 

Halmashauri ya Mpimbwe kwa sasa inapokea umeme kutoka Zambia ambao umeelezwa kukatika mara kwa mara kunakosababishwa na radi zinazopiga nguzo za umeme kwenye milima Lyambalyamfika inayotenganisha mkoa wa Rukwa na halmashauri ya Mpimbwe. 

Akizungumza wakati wa kukagua nguzo za umeme kwa ajili ya utekelezaji mradi huo katika wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema, uamuzi wa serikali kujenga njia ya umeme siyo tu utawasaidia wananchi na wafanyabiashara bali utachochea shughuli za maendeleo kwenye halmashauri ya Mpimbwe hususan wananchi wa jimbo lake la Kavuu. 

"Mama tunakushukuru sana sisi wananchi wa Mpimbwe na Mlele. Pia nimshukuru Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango alipotembelea kituo cha umeme Mlele alitoa maelekezo kuwa njia ya umeme kutoka Inyonga kwenda Majimoto ijengwe. Nashukuru sana na huo  ni ushahidi tosha kwamba sasa kazi imeanza utekelezaji". Amesema Mhe. Pinda 

"Wafanyabiashara wenye mashine za kukoboa mpunga na mazao memgine ya chakula wawe watulivu na baada ya miezi michache ni kama opereshemi ya miezi miwili tutakuwa tuna umeme, utakapowashwa ule wa gridi ya taifa maana yake utawashwa mpaka jimbo la Kavuu ambalo kadhia ya umeme inaenda kumalizika". Alisema. 

Naye mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mjengwa amemueleza Mhe, Pinda kuwa, tayari wameanza kupokea nguzo kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka  Inyonga hadi Majimoto halmashauri ya Mpimbwe wenye urefu wa takriban kilomita 135 ambapo ameelezea kuwa hatua hiyo ni faraja kwao na wananchi wa Mlele kwa ujumla na kwamba wao kama wasimamizi wa mradi watahakikishia mahitaji yote muhimu kama vile ulinzi kwa watakaofanya kazi kipande chote cha hifadhi unaimarishwa. .