National News

TBS NA ARSO WAWAKUTANISHA WATAALAMU WA AFYA NCHI 11

Tarehe: 08 Apr, 2024


SHIRIKA la Viwango Afrika (ARSO) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamewakutanisha wataalamu wa masuala ya afya kutoka nchi 11 barani Afrika kwaajili ya uandaaji viwango vya huduma za afya ili kuboresha huduma kwenye sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo 08 Aprili, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Sempeho Manongi amesema wamekutana kwaajili ya kuandaa, kujadili, na kuboresha viwango vya huduma za afya ili kuhakikisha wanalinda afya, mazingira na usalama katika bara la Afrika.

"Duniani kote, shughuli za wazalishaji na watoa huduma zimekuwa kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha ajira. Hivyo usalama wa walaji kupitia matumizi ya  viwango itasaidia  utambuzi wa bidhaa bora na salama kwa matumizi, na pia itapunguza athari ya matumizi ya bidhaa za huduma za afya sizisokidhi matakwa ya viwango". Amesema 

Aidha amesema kuwa bara la Afrika limeingia katika soko huru la Afrika (Africa free continental Trade) ambapo inalazimu kufanya shughuli za kibiashara kwa pamoja,na kwamba viwango vya namna hiyo ni muhimu kutokana na  shughuli zote za kiafya na bidhaa kutakiwa kuwa na viwango sawa huku akitoa rai kwa kamati ya kitalaam kuzingatia miongozo yote ya uandaaji viwango ili kupata viwango vinavyotekelezeka ambavyo vitasaidia bara la Afrika kupata faida za matumizi ya Viwango.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), Dkt. Hermogène Nsengimana amesisitiza viwango ambavyo vinaandaliwa viwe vinatekelezeka kwa kushirikiana na wadhibiti wa nchi zetu huku Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt.Athuman Ngenya akisema kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya afya barani Afrika zinaweza kuvuka mipaka ya nchi na kuhusisha masuala ya ubora, usalama, na upatikanaji wa huduma za afya.

"Ni jukumu letu kama wataalamu katika eneo hili kuhakikisha kwamba tunajenga mifumo imara ya viwango ambayo itasaidia kupunguza changamoto hizi na kuimarisha sekta ya afya kwa ujumla". Amesema Dkt. Ngenya.

Mkutano huo unafanyika kwa siku nne kuanzia 08 -11 Aprili, 2024 ambapo wataalamu hao wanatarajia kupata wazo la pamoja namna ya kuwa na viwango vya ubora wa huduma hiyo nyeti katika bara zima.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab