National News

JUA KUPATWA KIKAMILIFU LEO

Tarehe: 08 Apr, 2024


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema leo tarehe 8 Aprili,2024 kunatarajiwa kutokea kwa tukio la kupatwa kwa jua kikamilifu ambapo tukio hilo linatarajiwa kutokea upande wa bara la Marekani Kaskazini kupitia Mexico, Marekani na Canada.

Kupitia taarifa iliyotolewa na TMA, imesema hali ya kupatwa kwa jua ni tukio linalohusisha kivuli cha mwezi kuangukia juu ya uso wa dunia, ambapo katika maeneo yaliyo ndani ya kivuli hicho jua huonekana likifunikwa na mwezi kwa kipindi cha saa chache.

Sambamba na hayo pia tukio hilo linatarajiwa kuanzia maeneo ya kusini mwa bahari ya Pacific, na Mexico itakuwa nchi ya kwanza kufikiwa na kupatwa kwa jua kikamilifu majira ya saa 5:07 asubuhi kwa saa za Marekani. 

Aidha taarifa hiyo imeelesa kuwa njia ya kupatwa kwa jua itaendelea kutokea Mexico na kuingia Texas,  majira ya saa 7:40 mchana, ikipita baadhi ya maeneo kisha kuingia kusini mwa Ontario, Canada na kutoka bara la Marekani Kaskazini, kupitia pwani ya bahari ya Atlantiki, katika mji wa Newfoundland, Canada, saa 11:16 jioni.

Kwa kawaida, sehemu ya Jua inayofunikwa na mwezi wakati wa kilele cha kupatwa kwa jua kikamilifu itatofautiana baina ya eneo na eneo ambapo TMA imesema, kwa kuwa Tanzania inaangukia katika eneo la mbali zaidi na njia hiyo, haitashuhudia tukio hilo.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab