National News

YANGA WAIANDIKIA BARUA CAF

Tarehe: 06 Apr, 2024


Ikiwa imepita siku moja tangu itolewe katika michuano ya CAF Champions League hatua ya robo fainali katika mchezo dhidi ya Mamelod Sundowns, Klabu ya Yanga SC imeandika barua ya malalamiko kwa CAF kufuatia kukataliwa kwa goli la Azizi Ki dakika ya 58 pasipo refa wa mchezo huo, Dehane Beida, Raia wa Mauritania,  kwenda kujiridhisha katika VAR.

Kwenye barua hiyo ambayo Yanga imeiandika kupitia kwa Mkurugenzi wake wa sheria, Simon Patrick, imewalalamikia marefa kwa kushindwa kutumia teknolojia ya VAR kupata ufumbuzi, hivyo wanaamini na kulalamika kupitia sheria namba XVI kwamba kuna viashiria vya upangaji wa matokeo ikiwemo pia kitendo cha refa wa kati kushindwa kwenda kwenye VAR kuangalia utata wa goli hilo licha ya kwamba aliweza kwenda kwenye VAR kuhakiki faulo ya mchezaji wa Yanga.

Kwenye barua hiyo pamoja na mambo mengine Yanga wameiomba CAF ichunguze tukio hilo kwa undani kwa kutumia ushahidi wa rekodi za VAR na footage za mechi ili kubaini endapo kuna viashiria vya upendeleo kwa Mamelodi vimefanyika na ikijiridhisha kuna upendeleo ichukue hatua kwa kila aliyehusika, iweke hatua madhubuti za kudhibiti tukio kama hilolisijirudie kwenye mechi zijazo na pia ichukue maamuzi mengine ambayo CAF itaona yanafaa chini sheria ya mpira za CAF namba XVI, kifungu namba 3.