National News

KATA 22 TANZANIA BARA ZINAFANYA UCHAGUZI LEO

Tarehe: 20 Mar, 2024


Wananchi hii leo wanashiriki  zoezi la kupiga kura katika uchaguzi mdogo kuchagua wagombea 127 wa nafasi ya udiwani kutoka katika vyama 18 vya siasa hapa nchini kwenye kata 22 za Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele ameyasema hayo  jijini Dar es Salaam kuwa kati ya wagombea hao wanaume ni 89 huku wanawake wakiwa ni 38. 

Aidha amesema wapiga kura 128,157 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanashiriki katika uchaguzi huo mdogo huku jumla ya vituo 373 vya kupigia kura vikiwa vinatumika katika zoezi hilo ambapo pia ametoa pongezi kwa wadau wote wakiwemo wapiga kura na wananchi katika kata zote (22) zenye uchaguzi kwa utulivu waliouonesha wakati wote wa kipindi cha kampeni. 

Sambamba na hayo pia Jaji Mwambegele amefafanua kuwa
mawakala wanawajibika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao na katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu za uchaguzi na Maelekezo ya Tume.  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab