SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO SEKTA UHIFADHI WANYAMAPORI
Tarehe: 04 Mar, 2024
Serikali imejipanga kuboresha utendaji kazi, kuleta mapinduzi katika utoaji huduma na utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi wa Wanyamapori, ikiwemo utatuzi wa migongano baina ya binadamu na Wanyamapori.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani 4Machi 2024, yenye lengo la kuamsha ari na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu uhifadhi na umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali za Wanyamapori na misitu yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Stendi ya zamani, Wilayani Babati Mkoani Manyara.
Amesema Serikali imeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali za sekta hiyo za ujangili, biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu, uvamizi wa maeneo ya hifadhi, shoroba na mtawanyiko wa wanyamapori, kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi na mabadiliko ya tabia nchi.
Waziri Kairuki ameitaja mikakati hiyo kuwa ni Mkakati wa Kutekeleza Sera ya Wanyamapori wa Mwaka 2023 – 2033, Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili wa Mwaka 2023 – 2033, Mpango Mkakati wa Kupambana na Wanyamapori wakali na Waharibifu wa Mwaka 2020 – 2024, Mpango Mkakati wa Kuongoa Shoroba wa Mwaka 2022-2026 na Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Wanyamapori za Jamii wa Mwaka 2023 – 2033.
Ameongeza kuwa Serikali pia inaendelea kushirikiana na wadau wengine katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kuandaa na kutekeleza matamasha mbalimbali ya uhifadhi na utalii kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii nchini akitolea mfano wa tamasha lililofanyika Wilayani Same hivi karibuni - SAME UTALII FESTIVAL.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na -Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dastan Kitandula, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, CP Benedict Wakulyamba, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe ,Makamishna wa Uhifadhi wa TAWA, TANAPA, NCAA na TFS, Mkurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa kidini, Wakuu wa Idara na Taasisi, Maafisa na Askari wa Uhifadhi na Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii.