UHABA WA SUKARI WARUDISHA BIASHARA NYUMA, WATUMIAJI WAPUNGUZA KASI YA UNUNUZI
Tarehe: 26 Feb, 2024
Baadhi ya wafanyabiashara na watumiaji wa sukari katika manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma wameelezea namna uhaba wa sukari na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kulivyoathiri shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza na Main fm redio wamesema kuwa pamoja na athari nyingine pia imepelekea mzunguko wa bidhaa hiyo madukani kuwa mdogo ukilinganisha na kipindi cha nyuma kabla ya kutokea kwa changamoto hiyo.
Mmoja kati ya wafanyabiashara katika eneo la Mwanga anaeitwa Sogomba amesema kuwa wateja wakubwa wamepunguza kununua idadi kubwa ya mifuko ya sukari kutokana na kupanda kwa bei.
“Bei ya upandaji wa sukari inatuathiri kwa namna moja ama nyingine hasa kwa wateja wetu wakubwa unakuta mtu alikuwa na uwezo wa kuchukua mifuko mitano, mitatu, bei ikipanda…na sisi huwa hatuandaliwi kwahiyo mteja huwezi kumwandaa, vilevile anakuja ee bwana sukari bei gani, themanini na moja labda bei ya mwisho ilikuwa themanini kwahiyo hajajiandaa sasa badala ya kuchukua mifuko mitano nipe mifuko miwili nipe mmoja akienda huko nae mtumiaji wa mwisho labda alikuwa anachukua kilo tatu kilo tano atakuja kuchukua nusu, kilo”. Ameongeza Sogomba.
Mfanyabiashara mwingine Jacline Mwamba amesema;
“Inatuathiri wengi si mimi tu mfanyabiashara wa duka, hapana inatuathiri wote hata watumiaji, kwa mfano unakwenda kuchukua sukari dukani kwanza unaweza ukaenda ukakuta maduka mengi hamna sukari, sasa ukikuta duka moja lina sukari ambapo labda anaweza kuwa na mifuko kumi, ishirini anayo pekeyake karibia maduka kumi, ishirini yanayozunguka kwa eneo hilo unakuta nae anapandisha bei”. Ameeleza Jacline.
Sambamba na hayo pia wameiomba serikali kuchukua hatua kuhusiana na tatizo hilo la sukari kutokana na umuhimu wake katika maisha ya kila siku.
“Yaani sehemu ambayo sukari imekwama kama ni viwandani serikali itusaidie kama ni maswala ya miundombinu, kodi yaani serikali ituangalie wananchi wake kwasababu sukari ni muhimu sana kwa mwanadamu na hasa kwa sisi wenye watoto wachanga tunaathirika sana, wagonjwa kwasababu wanahitaji kupata vitu vyenye sukari na sukari imepanda” Amesema Jacline.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni serikali kupitia kwa Waziri wa kilimo Hussein Bashe imebainisha mikakati mbalimbali inayofanya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa sukari nchini pamoja na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ikiwa ni pamoja na kuedelea kuingiza sukari nchini kupitia kampuni iliyoingia makubaliano na NFRA.