National News

RAIS SAMIA ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA WALIOFARIKI KATIKA AJALI ARUSHA

Tarehe: 25 Feb, 2024


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za Rambirambi kwa familia za watu waliopoteza ndugu zao katika ajali iliyotokea jana iliyohusisha magari manne eneo la Ngaramtoni Arusha na kusababisha vifo vya watu 15.

Kupitia ukurasa wake wa "X" Rais Samia ameandika;

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 katika ajali iliyohusisha magari manne eneo la Ngaramtoni, mkoani Arusha.

Natuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliopoteza jamaa zao katika katika ajali hii. Ajali hizi zinachukuwa wapendwa wetu, nguvu kazi ya Taifa na mihimili ya familia. Naendelea kutoa wito kwa kila mmoja kuzingatia sheria za usalama barabarani katika matumizi ya vyombo vya moto. 

Naagiza vyombo vyetu vya ulinzi, usalama na udhibiti kuendelea kuhakikisha vinasimamia sheria kikamilifu, ikiwemo ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri na udhibiti wa leseni kwa madereva wanaorudia kuvunja sheria mara nyingi na wakati mwingine kusababisha watu kupoteza maisha.

Mwenyezi Mungu azilaze roho za ndugu zetu hawa mahali pema peponi. Amina" Samia Suluhu Hassan