National News

MILIONI 500 KUTOLEWA NA SERIKALI KUJENGA KITUO CHA AFYA PERAMIHO

Tarehe: 22 Jul, 2023


MILIONI 500 KUTOLEWA NA SERIKALI KUJENGA KITUO CHA AFYA PERAMIHO 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, Mhe. Angellah Kairuki ameahidi kuwa Serikali itatoa kiasi cha shilingi  milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Peramiho ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoyatoa mara baada ya Mbunge wa Peramiho Mhe. Jenista Mhagama kuwasilisha ombi la kujengewa kituo cha afya. 

Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo kwa wananchi wa Peramiho kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki, mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi hao. 

Mhe. Ndejembi amesema  kuwa kwa heshima na maelekezo ya Makamu wa Rais, fedha hiyo itatolewa mapema iwezekanavyo ili kuwezesha ujenzi wa kituo cha afya ambacho kitaboresha utoaji wa huduma za afya kwa jamii na kuongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho  unatokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Peramiho Mhe. Jenista Mhagama ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake.  

Pia amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni atapeleka gari mbili za kubebea wagonjwa katika Halmashuri ya Wilaya ya Songea, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa maboresho ya utoaji wa huduma za afya katika Hamashauri hiyo.  

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa mafanikio ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilayani Songea  na katika maeneo mengine yanajidhihirisha wazi kupitia kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya elimu ya awali, msingi na sekondari.
Chanzo:(OR:TAMISEMI)

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab