National News

SERIKALI IMEAJIRI WATUMISHI 18,418 WA AFYA NDANI YA MIAKA MITATU

Tarehe: 31 Jan, 2024


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Dkt. Festo Dugange amesema katika miaka mitatu  Serikali ya awamu ya sita  imefanya kazi kubwa  ambapo imeweza  kuajiri watumishi wa kada ya afya 18,418.

Aidha, kwa kipindi hicho serikali imegharimu sh.bilioni  195.3 kujenga miundombinu  ya Hospitali za Wilaya 136 na ukarabati wa hospitali kongwe 19.

Akizungumza Januari 31, 2014 kwenye uzinduzi  wa mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Dugange amesema serikali imejenga vituo vya afya 446  kwa sh.bilioni 718.18, ujenzi wa zahanati  955 kwa gharama ya Sh.bilioni 77. 41, majengo  ya dharura 80, wagonjwa mahututi  28 na nyumba za watumishi 150 kwa gharama ya sh. bilioni 45 ili kuboresha huduma za afya na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naibu Waziri Dugange akizungumzia wahudumu wa ngazi ya jamii, amesema ni watu muhimu ndani ya jamii kwa kuwa wao ndio daraja kati ya jamii na vituo vinavyotoa huduma za afya nchini ili wananchi wawe na afya njema.

"Kupitia mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ya jamii weledi na maarifa ya wahudumu hawa utaongezeka sambamba na wigo wa huduma wanazozitoa,"amesema.

Amesema Ofisi ya Rais Tamisemi ndio itakuwa na jukumu la  kusimamia zoezi la kuwapata wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakaojumuishwa kwenye mpango huo na tayari imeandaa taratibu na vigezo vya kuwapata wahudumu hao na mchakato wake utakuwa wa wazi ili  kuwapata  wanajamii wenye sifa na vigezo vinavyotakiwa. 
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania