National News

DARAJA LA CHUMA KUJENGWA MTO-NZUMBO KILOSA NZOLI

Tarehe: 29 Jan, 2024


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatarajia kuanza usanifu wa daraja la kudumu la chuma (Mabey Bridge) litakalojengwa ili kuunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo katika kata ya Ulaya-Mikumi Wilayani Kilosa.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff wakati akiongea na wananchi wa kata hiyo kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya miundombinu wilayani Kilosa.

“Nitawatuma wataalamu wangu wa TARURA Makao Makuu waje wafanye usanifu wa ujenzi wa daraja la kudumu la chuma ili kuunganisha vijiji hivi vya Nyali na Nzumbo”. Alisema 

Pamoja na hilo, amemwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro kuanza mara moja ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu (Kiteputepu) ili wananchi wa vijiji hivyo waendelee kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Vile vile Mhandisi Seff ameelekeza kufanyika kwa tathimini ya uharibifu wa barabara za Mikumi  ili ziwekwe kwenye mpango wa dharura wa kurudisha mawasiliano haraka iwezekanavyo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge - TAMISEMI Mhe. Dennis Londo amesema barabara nyingi za Jimbo la Mikumi  zimeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuiomba  TARURA kuangalia uwezekano wa kukarabati hasa barabara za Kivungu-Kilangali Km. 1.5, barabara ya Miyombo-Dodoma Isanga Km. 10 pamoja na ujenzi wa daraja la kudumu la Nyali-Nzumbo.

Daraja la watembea kwa miguu katika mto Nyali ambalo linaunganisha  vijiji vya Nyali na Nzumbo litajengwa kufuatia lile la awali kuvunjika.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab