National News

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA DINI

Tarehe: 27 Jan, 2024


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, leo amemwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu Jovitus Mwijage ikiwa ni tukio la kihistoria kutokana na kupita takriban miaka 50 kutoka kufanyika sherehe kama hiyo ya uwekaji wa wakfu. 

Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato.

Akitoa Salam za Dkt. Samia kwa waumini na wananchi waliohudhuria sherehe hizo, Dkt. Biteko ameeleza kuwa, Rais  ataendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ili kwa pamoja walete maendeleo nchini.

Amesema, Rais anatambua kuwa bado kuna changamoto mbalimbali nchini ambazo Serikali inafanya kila jitihada ili kuzindoa lakini hili litafanyika kwa ufanisi endapo hakutakuwa na mgawanyiko nchini kama ambavyo ilivyo sasa.

Ameeleza, Serikali inatambua kuwa kuna tofauti nyingi nchini ikiwemo za makabila na madhehebu lakini tunu inayounganisha watu wote ni haki, uhuru, umoja na amani ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi.

"Mheshimiwa Rais anatambua kutofautiana ikiwemo katika  mawazo  lakini kama mnavyojua kuwa amekuwa ni muumini wa maridhiano kwani anayaishi na anatoa nafasi kwa kila mmoja kutoa mawazo yake bila kubughudhiwa." Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amemtakia kila la heri Askofu Mwijage katika majukumu yake mapya kwenye kanisa na malezi ya jamii kwa ujumla na kueleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa  imani kuwa ni kiini cha ustaarabu na uungwana miongoni mwa jamii.

Ameongeza kuwa, kuwekwa wakfu kwa Askofu Mwijage kunatoa mafundisho mengi ikiwemo kutotanguliza hofu pale kunapotokea majukumu mapya kutokana na Askofu huyo kuwa tayari kutumikia  majukumu yake bila kuweka vikwazo mbele na kwamba hili ni somo kwa wananchi wengine kuwa tayari kutekeleza majukumu bila kutanguliza vikwazo.
#mainfmupdates

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab