National News

MKATABA HEWA UKAA WASAINIWA KIGOMA

Tarehe: 24 Jan, 2024


Serikali mkoani Kigoma imesaini mkataba kwa ajili ya  utekelezaji wa hatua za awali za Mradi wa Hewa ukaa unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika Halmashauri za wilaya Kakonko, Kibondo na Kasulu.

Mkataba huo utatekelezwa na Kampuni ya Orsted Nature Based Solution A/S kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Denmark (DRC) kwa kipindi cha Miaka 30 kuanzia Mwaka 2024, ambapo jumla ya hekta 500,000 zinatarajiwa kupandwa miti katika halmashauri hizo.

Akizungumza kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wakati wa kusaini mkataba huo, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza amesema sambamba na kuongeza kasi ya utunzaji wa Mazingira, mradi  utaongeza tija ya kiuchumi kwa wakazi mkoani Kigoma.

Amesema utekelezaji wa mkataba utafanyika kwa njia shirikishi ambapo kupitia mikutano, waratibu wa mradi watakutana na kukubaliana na wananchi hatua zote za utekelezaji wa mradi huo.

Mratibu wa Mradi Alfred Mageima amesema mradi umejikita katika  halmashauri hizo tatu za Mkoa kwa sababu ya uwepo wa kiasi kikubwa cha athari za uharibifu wa Mazingira kutokana na shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikifanywa na wakimbizi katika maeneo hayo.

Amesema mradi utazinufaisha halmashauri hizo kupitia fursa za kuwezeshwa kifedha ili kuimarisha miundombinu ya  kutolea huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule pamoja na vituo vya kutolea huduma za Afya.

Aidha mratibu huyo ameyataja malengo mahususi ya mkataba huo kuwa ni pamoja na kukubaliana na wananchi katika kutenga maeneo ya uhifadhi, kuhuisha na kuhifadhi misitu itakayotambuliwa pamoja na kuimarisha ulinzi wa maeneo tengefu.

"Ifahamike kuwa, katika halmashauri tulizozipendekeza, misitu imeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi makubwa ya miti kwa ajili ya nishati ya kupikia, ufugaji uliopitiliza pamoja na Kilimo cha kuhama hama. Hivyo kupitia mradi huu tutaimrisha hifadhi za misitu ili kudhibiti hewa ukaa katika maeneo hayo na Dunia kwa ujumla" amesema Alfred.
#kigoma #hewaukaa #kibondo #kakonko #kasulu
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab