WAZIRI MKUU MAJALIWA AITAKA NAM KUENDELEZA USHIRIKIANO MASUALA YA KIULINZI
Tarehe: 20 Jan, 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesisitiza Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) wahakikishe wanashiriki katika kila tukio la umoja huo pamoja na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo wakati akihutubia katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 - 20 Januari, 2024 ambapo anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.
“Tumezungumzia hali ya mabadiliko ya tabia nchi na namna tunavyopata athari kwenye maeneo yetu na umuhimu wa kuweka mkakati wa namna ya kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye maeneo yetu.”
Masuala mengine ambayo aliyawekea msisitizo katika mkutano huo ni pamoja na kutoa wito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuangalia ajenda za NAM na kuona namna ya kushirikiana na NAM katika kuzitekeleza.
Mkutano huo wa siku mbili ulianza jana Ijumaa, Januari 19, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Ruwenzori, Speke Resort Kampala nchini Uganda. Katika mkutano huo Rais wa Uganda alikabidhiwa rasmi uenyekiti wa kundi hilo.
Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan mwezi Oktoba, 2019. Mkutano huo haukuweza kufanyika tangu mwaka 2019 kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 lililoikumba dunia.