KIGOMA KUENDELEA KUISIMAMIA MIRADI MBALIMBALI YA MAENDELEO
Tarehe: 17 Jan, 2024
Serikali mkoani Kigoma imeahidi kuendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ili kuhakikisha malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi yanafikiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela wakati akizungumza kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Kakonko iliyolenga kukagua Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma pamoja na ile iliyo chini ya Halmashauri hiyo.
Amesema ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kielimu pamoja na Afya aliyoitembelea na kuikagua huku akiwapongeza viongozi pamoja na watendaji katika Halmashauri hiyo kwa kuhakikisha miradi inazingatia viwango na kukamilika kwa wakati kama ilivyoelekezwa na serikali.
"Nimeridhishwa na utekelezaji wa kazi mbalimbali kwani upande wa Miradi ya Elimu nimejionea hali halisi ya ukamilifu wa miundombinu ya madarasa, matundu ya vyoo pamoja na utoshelevu wa madawati hali inayoruhusu wanafunzi kusoma bila bugudha yoyote" amesema.
"Upande wa Afya pia nimejionea miundombinu imekamilika kama ilivyoelekezwa na serikali na ile inayoendelea kujengwa maendeleo yanaridhisha hivyo niwsisitize watendaji kuendelea kutoa huduma bora na yenye kuridhisha kwa wananchi" amesisitiza Msovela.
Aidha Katibu Tawala amesema Ofisi yake itaendelea kusimamia na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na Serikali mkoani hapa inalingana na thamani halisi ya fedha inayotolewa ili iweze kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.