National News

SERIKALI YAPIGA "STOP" SHUGULI ZA UVUVI ZIWA TANGANYIKA

Tarehe: 09 Jan, 2024


Baada ya miezi 8 kupita tangu kutolewa taarifa ya kusitishwa ufungaji wa Shughuli za Uvuvi katika Ziwa Tanganyika, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Abdalah Ulega ametangaza rasmi tena kusitishwa kwa shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika ili kulinda mazalia ya Samaki ambayo yanazidi kupotea huku akiwatoa hofu wavuvi kuhusu shughuli gani watakazofanya pale utekelezaji huu utakapoanza.

Pamoja na kuwa baadhi ya wavuvi wameonyesha kutokubaliana na agizo hilo lakini Waziri Ulega wakati akizungumza na kamati ya Uvuvi Mkoa wa Kigoma pamoja na viongozi kutoka Wizara hiyo amesema bila ya kusitisha shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika huenda mazalia yaliyopo hivi sasa yakatoweka kabisa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amesema wananchi hawana budi kupokea usitishwaji huo ili kulinda rasilimali zilizopo kwa ajili ya kizazi kijacho.

Mwaka jana mwezi Mei Serikali ilitangaza kusitishwa kwa shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika kwa kipindi Cha miezi 3, licha ya utekelezaji huo kutofanyika kutokana na mvutano uliokuwepo baina ya baadhi ya wabunge lakini pia wananchi wakihitaji kupatiwa shughuli mbadala pale shughuli za uvuvi zitakapositishwa.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab