National News

NDEJEMBI AWAPIGA STOP WATAALAMU MIFUMO IDARA YA UHASIBU UVINZA

Tarehe: 06 Jan, 2024


#Habari: Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Adolf Nduguru kuwabadilisha wataalamu wa mifumo wa idara ya uhasibu na kuwaleta wapya katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo kwenye nafasi zao.

Ndejembi ametoa agizo hilo baada ya kubaini kusuasua kwa ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.

Hatua ya kuwabadilisha wataalamu hao wa mifumo imekuja baada ya Mhe .Ndejembi kubaini kuwa changamoto iliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi ni idara ya uhasibu na fedha kushindwa kusimamia vizuri na kutatua tatizo la mfumo ambayo ilikuwa ndani ya halmashauri hiyo.

Naibu Waziri Ndejembi pia amemtaka Kaimu Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Philipo Marco kuhakikisha anasimamia ipasavyo ujenzi huo ili ukamilike kwa muda uliopangwa.

“ Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameleta fedha hizi Sh.bilioni tatu ili ziweze kunufaisha wananchi wa Kigoma na sisi wasaidizi wake hatutokubali kuona miradi hii inashindwa kutekelezeka tutawachukulia hatua watumishi hawa kwa kushindwa kusimamia miradi hii na naagiza pia ujenzi wa shule hii uanze kutekelezwa usiku na mchana leteni majenereta hapa kazi ifanyike hadi usiku,”amesema.

Amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kechegwa Masumbuko kuhakikisha kuwa kiasi cha fedha Sh. bilioni 1.8 iliyobaki inatumika ipasavyo na kumaliza sehemu ya kazi iliyobaki.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania