National News

"MASOKO YA JIONI YANACHANGIA UDUMAVU KWA WATOTO" - RC KIGOMA

Tarehe: 05 Jan, 2024


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema uwepo wa Masoko ya jioni unaendelea kuchangia kuwepo kwa changamoto ya udumavu na utapiamlo mkali kwa watoto mkoani humo.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo alipokutana na kuzungumza na wataalam wanaosimamia na kuratibu Mradi wa USAID-Lishe Mtambuka waliopo mkoani Kigoma kwa ajili ya  kutambulisha mradi huo, huku akisisitiza kuwa mkoa utaendelea kushirikiana na wadau wa Afya
katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Andengenye amesema baadhi ya wafanyabiashara hususani wanawake wamekuwa wakifanya shughuli zao kwenye masoko hayo hadi saa nne usiku na kushindwa kuandaa chakula kwa wakati hali inayosababisha watoto wao kulala bila kupata mlo wa usiku.

"Shughuli za kibiashara kupitia masoko haya ya usiku husababisha wazazi kukosa muda mzuri wa kuwaandalia chakula cha usiku watoto wao hivyo hulala bila kula huku baadhi yao huamka asubuhi kwenda shuleni bila kupata hata kifungua kinywa, hii ni hatari kwa Afya za watoto wetu" Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Pia Andengenye amewakumbusha wakazi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata chakula wanapokuwa  shuleni.

Upande wake Msimamizi wa Mradi huo kitaifa Dkt. Joyceline Kaganda amesema 
lengo la Mradi ni kuhakikisha  kina mama wanajengewa uwezo wa kuandaa na kuwalisha watoto chakula bora ili kukabiliana utapiamlo.

Amesema Changamoto kubwa hujitokeza pale watoto wanapofikia muda wa kutotegemea maziwa ya mama na kuanza kula chakula, ambapo wazazi huwapa vyakula hivyo bila kuzingatia makundi ya chakula bora na kuanza kuwasababishia hali ya udumavu.

Tunataka kuibadili jamii kifikra ili kila mtu aweze kufahamu visababishi vya changamoto ya hali ya utapiamlo mkali na udumavu katika jamii ili tuweze kuidhibiti.

"Mkoa wa Kigoma unavyakula vya kutosha tatizo kubwa ni wakazi kushindwa kula kwa kuzingatia makundi ya mlo kamili pamoja huku baadhi wakiuza vyakula hivyo na kukabiliwa na njaa baada ya muda mfupi" amesema Dkt. Kaganda.

Sambamba na mkoa wa Kigoma, Mradi wa USAID-Lishe Mtambuka unatekelezwa katika Mikoa ya Njombe, Katavi, Rukwa na  Songwe.
#mainfmupdates
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania