National News

MRADI WA UMEME WA JNHPP WAFIKIA ASILIMIA 94.78

Tarehe: 28 Dec, 2023


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, utekelezaji wa  mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 kwa sasa umefikia asilimia 94.78 huku mashine mbili za kuzalisha umeme zikiwa tayari zimeshafungwa kwa ajili ya kuanza kuzalisha umeme.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 28 Desemba 2023 wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi huo wilayani Rufiji akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati aliyoteua Rais ya ufuatiliaji mradi wa JNHPP, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

“ Hatua iliyopigwa ya utekelezaji wa mradi huu kila mtu ameona kuwa ni kubwa kwenye hatua zote, mfano kwenye ujazaji maji wa bwawa la kuzalisha umeme, maji yamejaa kwa kiwango ambacho yanaruhusu kuzalisha umeme, pia ufungaji wa mashine ambazo zitatumika kuzalisha umeme, nafurahi kusema kuwa mashine mbili zimeshafungwa ambazo ni mashine namba Tisa na namba Nane na tunaamini kwamba mashine nyingine zitaendelea kufungwa kadri muda  unavyoenda ili kupata megawati zote 2,115.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, kufungwa kwa mashine hizo mbili kunatoa matumaini ya kutekeleza agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kupunguza changamoto za umeme nchini ndani ya miezi Sita ambapo sasa imebaki miezi mitatu ya utekelezaji wa agizo hilo kwani mashine hizo zitazalisha megawati 470 na kuingizwa katika gridi ya Taifa ili kuongeza kiwango cha umeme.

Ameeleza kuwa,  mashine namba Tisa itakapofika tarehe 2 Januari majaribio ya kwanza yajulikanayo kama dry testing yatakuwa yamekamilika na ifikapo mwezi Februari  tarehe 19 majaribo ya pili yajulikanayo kama wet testing yatakuwa yamekamilika tayari kwa kuanza kuzalisha umeme na kwa mashine namba Nane matarajio ni kuwa, na yenyewe majaribio yakamilike mwezi Februari 2024.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania