National News

"MABORESHO YA MIUNDOMBINU YAIMARISHE UCHUMI"- RC ANDENGENYE

Tarehe: 19 Dec, 2023


Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wananchi kuendelea kutumia vizuri fursa zitokanazo na maboresho ya  miundombinu mbalimbali yanayofanywa na Serikali ili kujiletea Maendeleo wao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Andengenye ametoa wito huo alipozungumza na wakazi wa Wilaya ya Kakonko alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Stendi ya Mabasi katika wilaya hiyo.

"Miundombinu tuliyonayo ambayo pia  tunaendelea kuitumia ndiyo maendeleo yenyewe hivyo tuitumie vizuri ili iweze kutunufaisha sisi na kizazi chetu kijacho" Amesema Rc Andengenye. 

Hata hivyo Andengenye amewakumbusha wakazi wilayani humo kuendelea kutunza amani kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Naye Mkuu wa Wilaya  ya Kakonko Kanali Evance Mallasa amesema uwepo wa masoko ya jioni wilayani humo unachangia kuathiri malezi bora na Maendeleo ya kitaaluma kwa watoto.

Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatumia wanafunzi kwenye shughuli za uzalishaji mali katika muda ambao wanatakiwa kuwepo  darasani.

"Ninaunga mkono katika kuwajengea watoto stadi za maisha lakini kila jambo lifanywe kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyopo, vinginevyo tutakuwa hatuwapatii haki zao za kimalezi watoto wetu" amesisitiza Mallasa.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kakonko Ndaki Mhuli amesema mradi huo wa ujenzi wa stendi unatekelezwa kwa Thamani ya Shilingi Bil. 3.5 kutoka serikalini na unatarajia kukamilika ifikapo Januari 23, 2024.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab