National News

KIGOMA YATWAA TUZO MZALISHAJI WA PILI MAZAO YASIYONAFAKA

Tarehe: 13 Dec, 2023


Mkoa wa Kigoma umepokea Tuzo ya Mzalishaji wa Pili wa Mazao yasiyonafaka 2022/2023 iliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwenye kilele cha Maonesho ya kimataifa ya Kilimo Biashara 2023.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema tuzo hiyo ni matokeo chanya  ya utekelezaji mzuri wa Sera za Kilimo zinazoratibiwa na kusimamiwa kwa ufasaha na Wizara ya Kilimo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu.

Amesema kimkoa msingi wa kuyafikia  mafanikio hayo ni upatikanaji wa uhakika wa mbolea ya ruzuku, kusogezwa kwa huduma za ugani pamoja na wananchi kuwa tayari kupokea mabadiliko na kuanza kujikita katika mfumo wa Kilimo cha kisasa na chenye tija.

"Kwetu sisi tuzo hii ni deni kwani tunaahidi kuongeza kasi ya uzalishaji ili kuweza kulisha viwanda vyetu kwa bidhaa za ndani na kupunguza gharama ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na sisi kugeuka wauzaji katika soko la Dunia ili kukuza uchumi wa taifa" alisema.

"Nitoe wito kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma kuendelea kutumia kwa ufasaha na uaminifu  fursa ya ruzuku inayoelekezwa kwenye Sekta ya kilimo upande wa Mbolea na Pembejeo za Kilimo ili tupate matokeo chanya kiuzalishaji badala ya kunufaisha watu wachache ambao sio walengwa kwa kuuza pembejeo hizo" alisisitiza  Andengenye.

Mkuu wa Mkoa amewakumbusha wakulima kuendelea kuzingatia misimu ya kilimo, maelekezo ya wataalam wa kilimo pamoja na utunzaji mzuri wa mazao  mara baada kuvuna.

Pia Andengenye ameishauri jamii kuachana na Kilimo cha kuhama hama badala yake izingatie ushauri wa wataalam kupitia upimaji wa Afya ya udongo na kutambua mbolea sahihi inayohitajika kurejesha rutuba kuendana na mahitaji ya mazao, jambo litakalosaidia katika utunzaji wa mazingira ikiwemo uhifadhi wa misitu.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amebainisha  kuwa uongozi wa mkoa umedhamiria  kuhakikisha unaweka msukumo katika kuwajengea uwezo na kuwaingiza vijana wengi kwenye mfumo wa kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kutengeneza mazingira   yatakayoruhusu vijana kujiajiri kupitia Kilimo.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab