National News

WATATU WAKAMATWA KWA TUHUMA WIZI WA PIKIPIKI

Tarehe: 11 Dec, 2023


#Habari: Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za wizi wa Pikipiki katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Akizungumza na waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma leo Desemba 11, 2023 ACP Filemon Makungu amesema watu hao wamekamatwa katika operesheni iliyofanyika Novemba 30, 2023 maeneo ya Mwasenga, Manispaa Kigoma Ujiji.

"Askari wakiwa doria waliwakamata watuhumiwa watatu wanaojihusisha na matukio ya wizi wa Pikipiki mkoani humo wakiwa na pikipiki 01 yenye namba za usajili MC 976 DRQ aina ya Kinglion ambayo ni mali ya wizi." amesema ACP Makungu.

Katika hatua nyingine Makungu pia amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Nchi ya Burundi wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja raia wa Tanzania akijaribu kuvuka mpaka kuelekea Burundi akiwa na pikipiki yenye namba za usajili MC 429 DMU aina ya Kinglion inayodhaniwa kuwa mali ya wizi.

Aidha ACP Makungu amesema watuhumiwa wote wanaoshikiliwa na jeshi hilo watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika huku pia wakiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kuzuia na kubaini uhalifu na wahalifu kwa lengo la kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania