SERIKALI KUENDELEA KUIUNGA MKONO (TIA) KATIKA MIPANGO YAKE
Tarehe: 02 Dec, 2023
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Hamis Kalli amesema kuwa serikali itaendelea kuunga mkono katika kufanikisha programu mbalimbali ambazo chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) kinatekeleza ili kuhakikisha kuwa kinaendelela kuwa bora zaidi.
Kalli ameyasema hayo leo 1 Novemba 2023 wakati akitoa hotuba kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipomwakilisha kama mgeni rasmi katika mahafali ya 21 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Kigoma ambapo ni mahafali ya kwanza kufanyika katika mkoa wa Kigoma.
"Niwahakikishie serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwaunga mkono ili muweze kufanikisha program mnazoziandaa Pamoja na ujenzi huo kuusimamia ili uweze kukamilika na vijana waweze kuhamia pale,ndugu mwenyekiti nimefurahishwa sana na mpango wa ukuzaji na uendelezaji wa vijana kitaaluma na kitaalamu yaani Carrier Development Program, nimeona mwenyewe na nimefanya utafiti kwa wanafunzi nimeona vibanda wanafunzi wameweza kujitoa wanachuo na kuonyesha kufanya elimu kwa vitendo kumbe sasa chuo hiki ni chuo kinachotembea" amesema Kalli
Kwa upande wake Afisa mtendaji mkuu Taasisi ya Uhasibu Tanzania TIA Prof. William Pallangyo amesema kuwa kampasi hiyo ya Kigoma imeanza kuendesha madarasa kwaajili ya maandalizi ya mitihani ya bodi ya taifa ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu Tanzania.
"Kampasi ipo katika ujenzi wa majengo yake ili kuhama katika majengo ya kupanga, ujenzi huo unaendelea katika Kijiji cha Kamala kata ya Mungonya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na ujenzi unajumuisha kumbi za mihadhara, madarasa kumi yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 1000, maktaba, maabara ya kompyuta pamoja na ofisi 25 za watumishi.
Pia profesa Pallangyo amesema kuwa ujenzi wa majengo hayo umeanza tangu Juni 15, 2023 na utarajiwa kukamilika Disemba 14,2024 ambapo mradi huo unagharamiwa na serikali ya awamu ya sita na hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi Bilioni 11 Milioni 80 na laki saba 35 elfu, na 67 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 25% na katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 910 wametunukiwa vyeti vyao.