National News

MAJALIWA ATOA AGIZO KUWASAKA WANAOTUHUMIWA KUWAPA UJAUZITO WATOTO WAKIKE MKOANI SONGWE

Tarehe: 24 Nov, 2023


#Habari: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo akiwa mkoani Songwe kwa ziara ya siku 3 amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa huo Dkt. Francis Michael na Wakuu wa Wilaya zote za mkoa huo kuhakikisha wanawasaka watu wote wanaotuhumiwa kuwapa mimba watoto wa kike.
 
“Tangu Januari hadi sasa, mkoa huu una kesi 59 za wasichana walioacha shule kwa sababu ya ujauzito lakini ni kesi mbili tu zimeeenda mahakamani. Hizo 57 ziko wapi au zimeishia wapi? Ni nani anazuia kesi hizi zisiende? Jeshi la Polisi, ni kwa nini hatuwafikishi watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria?, amehoji.
 
“RC na Ma-DC wote kaeni na Kamati zenu za Ulinzi mbainishe wahusike na mhakikishe hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika,” amesema Waziri Mkuu leo (Alhamisi, Novemba 23, 2023) wakati akitoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana Ileje.
 
Amewakemea vijana wanaopenda kutembea na watoto wa shule waache tabia hiyo mara moja kwani wanakatisha maisha ya baadaye ya watoto hao. “Sheria iko wazi katika kosa hili. Adhabu yake ni miaka 30, kijana kabla hujamfuata binti jiulize una miaka mingapi, sababu tukikufunga utarudi ukiwa mzee,” amesema.
 
Akisisitiza haja ya kuwalinda mabinti, Waziri Mkuu amesema: “Hawa ni watoto wetu, tunapaswa tuwalee ili wakue na kuja kushika majukumu ya nchi Rais Samia amewekeza kwao kwa kutoa elimu bila ada tunapaswa tuhakikishe wanatimiza ndoto zao, kwa hiyo tuwalee ili waweze kuhitimu,” amesisitiza.
 
Amewaomba masheikh na wachungaji wakemee tabia hiyo kupitia mahubiri ya kwenye ibada.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapongeza wana-Ileje kwa kujenga maabara ya kompyuta kwenye shule hiyo yenye mikondo ya kidato cha kwanza hadi cha nne ili kuhimiza matumizi ya TEHAMA.
 ..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
www.mainfm.co.tz
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania