National News

MAAFISA UVUVI WATAKIWA KUONGEZA KASI KUDHIBITI KUENEA ZANA HARAMU ZA UVUVI

Tarehe: 18 Nov, 2023


Maafisa Uvuvi mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza kasi katika kudhibiti kuenea kwa zana haramu za uvuvi kabla ya kununuliwa na wananchi ili kuwaepushia hasara kutokana na zana hizo kukamatwa na kuteketezwa na Serikali.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Alexander Mnyeti  alipozungumza kwenye hafla  ya kukabidhi boti tisa za kisasa za uvuvi kwa wanufaika mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa lengo la serikali kupitia wizara hiyo ni kuimarisha uchumi wa wananchi kwa kuhamasisha na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya Samaki.

Mnyeti amesema maafisa uvuvi wanapaswa kufuatilia na kuhakikisha wanafunga maduka kisha kuwakamata wafanyabiashara wote  wanaouza nyavu ambazo kisheria haziruhusiwi kutumika kwa shughuli za uvuvi.

"Naagiza nendeni mkafanye msako katika maeneo yote yanayozalisha, kuuza au kufanya matumizi ya zana harama za uvuvi na kuzidhibiti ili zisiweze kutumika katika mito, mabwawa, maziwa na bahari zetu." ameagiza Mnyeti.

Aidha Naibu Waziri amewakumbusha watendaji hao wa serikali kutekeleza majukumu yao kutoa elimu na miongozo ya uvuvi bora na wa kisasa badala ya kusubiri wavuvi wafanye makosa ili kuwatoza fedha kutokana na makosa hayo na kusababisha baadhi yao kufilisika.

"Baadhi yenu mmegeuka wakusanya mapato wa Halmashauri badala ya kusimamia majukumu yenu ya msingi ikiwemo kutoa elimu na kusimamia taratibu za uvuvi wa kisasa" amesema Mnyeti.

Baadhi ya wanufaika wa boti hizo zilizotolewa kwa njia ya mikopo nafuu kutoka serikalini wamesema wanauhakika wa kurejesha  mikopo yao kutokana na vyombo hivyo kutumia mifumo ya kisasa katika mchakato wa uvuvi.

Jumla ya boti tisa zenye thamani ya Shilingi 535 Milioni zimekabidhiwa kwa vikundi vya wanufaika katika Halmashauri za Kigoma, Uvinza  na Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mnyeti amemaliza kwa kusema kuwa Ziwa Tanganyika lina samaki wengi lakini  kubwa ilikuwa matumizi ya zana duni za uvuvi na zilizopitwa na wakati na hivyo matumizi ya zana mpya yatasaidia sana katika shughuli za uvuvi.
cc:kigomars 
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab